TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA HII INATOLEWA NA MASHIRIKA YA KIRAIA KUELEZEA MSIMAMO WAO KATIKA KAMPENI INAYOENDESHWA NA MTANDAO WA AVAAZ KUHUSU KUTAKA SERIKALI KUSIMAMISHA MCHAKATO WOWOTE WA KUUZA ENEO LA LILIONDO KATIKA MFUMO WA IKOLOJIA YA SERENGETI UPANDE WA MASHARIKI AMBAYO NI ARDHI YA VIJIJI
SISI mashirika ya kiraia yanayofanya kazi nchini Tanzania katika masuala ya haki za binadamu, uchumi wa kijamii, ikiwa ni pamoja na ardhi, usawa wa kijinsia, mazingira na rasilimali kwa jumla tunaunga mkono kampeni inayoendeshwa na mtandao wa kimataifa wa Avaaz ambao ni ulingo wa kimtandao unaotetea haki za binadamu kwa njia ya matamko mbalimbali. Mtandao huu umetoa wito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusitisha mpango wowote wa kuuza ama kutoa sehemu ya ikolojia ya mashariki ya hifadhi ya Serengeti ambayo ni makazi ya wafugaji wa Kimaasai katika wilaya ya Ngorongoro, tarafa ya Loliondo kwa kampuni ya uwindaji wa wanyama pori ya OBC. OBC ni kampuni ya uwindaji inayomilikiwa na familia ya kifalme ya Ufalme wa Umoja wa nchi za Kiarabu (United Arabs Emirates - UAE). Itakumbukwa kuwa mitandao ya Tanzania Land Alliance (TALA) na FEMACT imekuwa ikijishughulisha na migogoro ya Loliondo kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kutoa matamko mbalimbali. Hata hivyo, serikali imekuwa ikisita kutekeleza mapendekezo hayo.
Mgogoro wa Loliondo umekuwepo kwa takriban miaka 20 tangu mwaka 1992 lakini ilifikia kilele mwaka 2009 ambapo serikali iliwatoa kwa nguvu wafugaji wa kimaasai katika eneo la ikolojia ya Serengeti upande wa mashariki kwa lengo la kuanzisha korido au mapito ya wanyama pori katika eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,500 ambalo ni ardhi ya vijiji saba (7) vya Loliondo. kwa kuanzishwa kwa mapito ya wanyama katika enelo hilo, maisha ya watu takriban 48,000 yataathirika na mifugo mingi pia.
HISTORIA FUPI YA UWEKEZAJI KATIKA ENEO LA MGOGORO, LOLIONDO
Tangu eneo la Loliondo ambalo ni eneo la ikolojia ya Serengeti kwa upande wa mashariki kupewa mwekezaji wa Kiarabu ambaye ni familia ya Kifalme kutoka nchi za Umoja wa Kifalme za Kiarabu kupitia kampuni ya OBC (Otterlo Business Corporation) mwaka 1992, eneo la Loliondo liliendelea kuwa na mgogoro baina ya vijiji kwa upande mmoja na OBC na serikali kwa upande wa pili. OBC walipewa kibali cha uwindaji katika eneo lote la Tarafa ya Loliondo na Sale wilayani Ngorongoro tangu mwaka 1992. Tangu wakati huo ambapo kampuni ya OBC inapewa kibali cha uwindaji, kulizuka upinzani wa wananchi kutokana na mchakato wa kumpa OBC eneo la kuwindia kutokuwa wazi na pia shirikishi. Kutokana na mapungufu haya baina ya serikali na OBC, ulizuka mgogoro ambao umeishi mpaka leo bila ufumbuzi. Hata hivyo, mwaka 2008 serikali wakishirikiana na OBC waliandaa mkataba na vijiji, mkataba huo ulitaka vijiji kuondoka kwa hiari katika eneo hilo ambalo OBC wameweka kambi yao ili kuweza kufanya uwindaji wa kibiashara. Katika mchakato huo wa mikataba, vijiji vingine vilikubaliana na vingine vikakataa. Kutokana na kutokubalika kwa mikataba hiyo kwa asilimia zote, serikali mwaka 2009 July iliazimia kuwatoa wamasai katika eneo hilo kwa nguvu jambo lililopelekea jamii ya wafugaji wa kimaasai kupata hasara kublwa ikiwa ni pamoja na kunyimwa kulisha na kunyesha mifugo yao katika eneo hilo. Tangu kumalizika kwa operesheni hiyo, serikali iliendelea kufanya michakato mbalimbali kuhusiana na eneo hilo yenye malengo ya kufanikisha azma yao ya kuhakikisha kuwa eneo hilo linatengwa kutoka katika ardhi ya vijiji na kuachwa chini ya Kampuni ya Kiarabu, OBC kwa ajili ya utalii wa Uwindaji.
MADHARA YATOKANAYO NA WANANCHI KUONDOLEWA KWA NGUVU LOLIONDO MWAKA 2009
Kutokana na operesheni ya kuwaondoa wananchi, wafugaji wa kimaasai katika ikolojia ya serengeti ilipitisha biashara ya uwindaji kwa kampuni ya OBC, wananchi waliathirika kwa kiasi kikubwa na yafuatayo ni baadhi tu ya madhara walioyapata;
- Usumbufu kwa wananchi;
- Zaidi ya nyumba za wamasai 350 zilichomwa mtoto na kuteketea kabisa;
- Zaidi ya watu 20,000 walikumbwa na mkasa huo na kuondolewa kwa nguvu,
- Zaidi ya asilimia hamsini (50%) ya mifugo iliyokuwepo katika eneo hilo ilikufa kutokana na kukosa malisho ya kutosha na maji;
- Baadhi ya watoto walipotea wakati wa operesheni;
- Kuharibika kwa mimba za akina mama kutokana na hofu na mshtuko;
- Watu wengi kuchapwa na kudhalilishwa na kijana Ngodidyo Roriken alipigwa risasi ya jicho na kusababishiwa ulemavu wa jicho moja;
- Watu wengi walishitakiwa na kubambikiziwa kesi ya kuingia eneo la liliodaiwa la OBC angali ni eneo la vijiji.
HATUA ZILIZO CHUKULIWA NA SERIKALI BAADA YA OPERESHENI
Pamoja na operesheni kushindwa kuwaondoa wananchi katika eneo hilo, serikali iliendelea kuhakikisha kuwa inatimiza azma yake ya kutenga eneo hilo, kwa manufaa ya OBC. Baadhi ya michakato ambayo serikali iliendelea nayo baada ya operesheni ni pamoja na;
- Kutuma tume mbalimbali kuchunguza mgogoro bila kutoa wala kueleza matokeo ya uchunguzi wa tume hizo kwa umma wala kwa mamlaka husika.
- Mwaka 2010, serikali kupitia kwa Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro iliandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ya wilaya, mpango ambao ulilenga kutenganisha ardhi ya vijiji na eneo la ikolojia ya Serengeti na kuanzisha korido ya wanyama ambayo itakuwa ikitumiwa na OBC kuwinda wanyama. Mpango huu ulikataliwa na wananchi kupitia baraza la Madiwani, kwani haukuwa shirikishi na ulikuwa vigumu kuanzisha mpango wa matumizi bora ya ardhi ya wilaya kabla ya mipango ya vijiji kutengenezwa.
- Mwaka 2011, serikali iliandikia vijiji vyenye vyeti vya ardhi ya vijiji, vya Ololosokwan na Ngaresero barua na kuziraka kurudisha vyeti vyao ili kuvibatilisha kwa lengo la kufanikisha na kurahisisha uundaji wa korido ya wanyama.
- Kuanzishwa kwa mpango wa kuwatumia viongozi ndani ya jamii kuhamasisha jamii kuondoka ili kupisha serikali kuanzisha korido ya wanyama. Jamii kupitia mikutano yao vijiji vilikataa mpango huu baadhi ya viongozi kutumika na serikali na OBC kutaka kuwahamisha wananchi katika eneo hilo la ikolojia ambalo ndilo eneo la malisho ya mifugo kwa miaka mingi.
- Kutokanaa na michakato hiyo yote kuonekana kushindikana, bado serikali haijatolea uamuzi mgogoro huu, jambo linalosababisha wananchi kuishi kwa hofu kubwa bila kufahamu hatima ya maisha yao.
MAPENDEKEZO
Kutokana na hayo, sisi mashirika yanayojishughulisha na utetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania tunaunga mkono kampeni za mtandao wa kimataifa wa Avaaz na kuitaka serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya yafuatayo:-
- Kuacha mara moja mpango wa kuigawa ardhi ya vijiji kwa ajili ya kuanzisha korido ya wanyama kwa malengo ya kuwanufaisha wawekezaji wa OBC.
- Serikali iandae mpango shirikishi wa matumizi bora ya ardhi utakao zingatia maslahi na mahitaji ya wanavijiji wote.
- Mikataba yote inayohusu shughuli za uwindaji katika eneo husika iangaliwe na kuridhiwa upya ili kuzingatia haki, matakwa na maslahi ya wananchi juu ya rasilimali husika.
- Mapendekezo ya Kamati na Tume mbalimblai ziliotembelea eneo hilo yawekwe wazi na kutekelezwa ili tija ya matumizi ya kodi za wananchi ionekane.
- Serikali iache tabia ya kutumia nguvu kila wakati kunapokuwa na mvutano ama mgongano wa maslahi kati ya wananchi wa wawekezaji.
TALA FEMACT
NGONET PINGOS FORUM
MATUKIO KATIKA PICHA
Mwakilishi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP/FemACT Ndugu Neema Duma, akisoma taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani).
Mkurugenzi Mtendaji wa HAKIARDHI Yefred Myenzi akitoa ufafanuzi juu ya taarifa hiyo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)
Bwana Shilinde Ngalula - Wakili kutoka kituo cha sheria na haki za Binadamu (LHRC) akijibu maswali ya wanahabari (hawapo pichani) kuhusiana na msimamo wa mashirika ya kiraia kuitaka serikali kuacha mpango wa kuigawa ardhi vijiji katika eneo la Loliondo, Kulia ni Mkurugenzi wa shirika la PINGOs Forum Edward Porokwa akifuatilia kwa karibu.
Mratibu wa Mashirika ya Kiraia wilaya ya Ngorongoro Samwel Nangiria, akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa ufafanuzi juu ya taarifa ya msimamo wa mashirika hayo kuhusiana na eneo la Loliondo.
Imewekwa na Khadija Abdallah - ORS FM
Picha na Gideon John - ORMAME
No comments:
Post a Comment